Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua ujenzi wa Skuli mpya ya Msingi ya Mwanakwerekwe C unaogharamiwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa Chinankwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 1.6.
Kushoto ya Makamu wa Pili ni Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bibi Sheen Limun na Nyumba yake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mh. Ali Juma Shamhuna.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Ujenzi ya Fujian Group Company ya China Bw. Xiong Kaihua akimpatia maelezo ya ujenzi kwenye ramani ya Skuli mpya ya Msingi ya Mwanakwerekwe C Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Skuli hiyo inajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China ikiwa ya pili ikitanguliwa na ile ya Kijichi iliyoko Wilaya ya Magharibi
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bibi Sheen Limun akimkabidhi madeski 480 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi yaliyotolewa na Serikali ya Jimbo la Sichuani kwa gharama za Yuan za Kichina Milioni Moja.
Hii inafuatia ziara ya Balozi Seif Jimboni humo Mwaka jana kuhudhuria tamasha la 12 la Maonyesho ya Kibiashara huko Sichuani akimuwakilisha Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa misaada yake mikubwa inayotoa katika kuunga mkono harakati za Kiuchumi na Maendeleo za Zanzibar.
Shukrani hizo zimetolewa na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika sherehe za uzinduzi wa Ujenzi wa Skuli mpya ya Msingi ya Mwanakwerekwe C kwa ufadhili wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.
Uzinduzi huo umekwenda samba mba na Ubalozi wa China kukabidhi Madeski 480 ahadi ya Serikali ya Jimbo la Sichuan Nchini China wa Yuan Milioni Moja kuipatia Zanzibar kufuatia ziara ya Balozi Seif Jimboni humo Mwezi Oktoba mwaka 2011.
Balozi Seif alisema Madeski hayo yatasaidia kupunguza uhaba wa Vikalio kwa Wanafunzi wa Skuli mbali mbali hasa zile za msingi za Unguja na Pemba.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mipango yake ya Maendeleo suala la Elimu limepewa nafasi ya pekee lengo likiwa ni kuona watoto wote wanapata fursa ya Elimu katika mazingira bora.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Bibi Sheen Limun kwa juhudi zake za kuunganisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Nchi yake na Zanzibar.
Alisema Balozi Sheen tokea amefika Nchini kuanza kutekeleza majukumu yake amekuwa chachu ya Maendeleo ya Zanzibar hasa katika Sekta ya Elimu.
Balozi Seif amewahimiza Wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali kupitia washirika wa maaendeleo katika kuimarisha sekta hiyo muhimu kwa Taifa.
Aliwataka Wanafunzi hasa wale wa Kiume kuacha mzaha katika kutafuta elimu vyenginevyo watakuja jikuta wakiongozwa na akina mama katika nyadhifa mbali mbali za utumishi wa umma.
“Bila ya elimu hakuna maendeleo yoyote yale. Taifa kukosa wataalamu mara zote zinakuwa butu. Tunashukuru sana kwamba Zanzibar haiko huko. Lakini hata hivyo vijana hasa wa kiume mnapaswa kuacha mzaha katika kusaka Elimu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akitoa nasaha zake Balozi mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Bibi Sheen Limun alisema China wakati wote itazidi kuongeza nguvu zake kwa Zanzibar katika kujenga mazingira bora ya Kielimu.
Bibi Sheen aliwahakikishia wanafunzi wa Zanzibar kwamba jitihada zinazochukuliwa na Serikali kupitia marafiki zitasaidia kuwajengea mazingira mazuri ya elimu wanafunzi hao.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali Bibi Mwanaidi Saleh alisema Ujenzi wa Skuli hiyo mpya ya Mwanakwerekwe C ulioanza mwezi huu unatarajiwa kukamilika Mwezi Marchi mwaka ujao wa 2013.
Bibi Mwanaidi alifahamisha kwamba Jengo hilo litakalogharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 1.6 litakuwa na Madarasa 12, Ofisi ya Mwalimu Mkuu, Maktaba na Chumba cha Kompyuta.
Ujenzi huo unaogharamiwa na Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China ni wa pili ukitanguliwa na ule wa Skuli ya Msingi ya Kijichi iliyoko Wilaya ya Magharibi.
Jumla ya Skuli 13 za Msingi Unguja na Pemba zimefanikiwa kugaiwa madeski hayo 480 kutoka msaada wa Serikali ya Jimbo la Sichuan Nchini China.
Skuli hizo ni pamoja na Bububu, Ukongoroni, Makadara, Karume Donge,Kitope, Kijichi, Matetema, Charawe, Donge Mtambile, Muembe Shauri, Rahaleo, Karange na Kidagoni.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/8/2012.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako/ Leave your comments