Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi akielezea umuhimu wa kuimarishwa kwa Karakana Kuu ya
Serikali iliyopo Chumbuni mbele ya Mkuu wa Karakana hiyo Nd. Mahmoud
Hassan Khatib kufuatia ziara yake ya ghafla kwenye Karakana hiyo.
Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Magari Zanzibar Nd.
Masoud Saadala akielezea changamoto zinazoikabili Taasisi yao katika
utekelezaji wa kazi zao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara ya ghafla katika karakana Kuu ya
Serikali iliyopo Chumbuni Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi akipata maelezo ya utendaji kazi kutoka kwa wahandisi wa
Karakana Kuu ya Serikali iliyopo Chumbuni kutoka kwa Mkuu wa Karakana hiyo Nd. Mahmoud Hassan Khatib.
Serikali kupitia
Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano inakusudia kuijengea uwezo zaidi
Karakana Kuu ya Serikali kwa lengo la kuirejeshea hadhi yake ya kutoa
huduma za kitaalamu zaidi.
Kauli hiyo
imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alipofanya ziara ya ghafla katika Karakana hiyo iliyopo Mtaa wa Chumbuni
Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema
haipendezi kuona vyombo vya Moto hasa vile vya Serikali vinapelekewa
kupata huduma ya kiufundi katika Karakana binafsi wakati ile iliyowekwa
Maalum na Serikali kwa ajili ya Vyombo hivyo inakiukwa.
Alisema mpango huo ambao sio utaratibu unaokubalika Kiserikali unaweza kutoa mwanya kwa baadhi ya watendaji wa Serikali kutumia vibaya Fedha za Umma katika utengenezaji wa vyombo hivyo.
“ Haitoi sura nzuri
kuona Maafisa wa Taasisi za Umma wanaamua kupeleka magari yao katika
karakana za nje wakati ile ya Serikali ipo kwa ajili ya shughuli hiyo”.
Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa Karakana hiyo kwamba lile
ombi lao lililopelekwa ngazi ya juu kwa ajili ya kupatia ufumbuzi
litaangaliwa Serikalini na kupatiwa ufumbuzi unaofaa.
Alisema hatua hiyo
itaweza kusaidia kwa njia moja Karakana hiyo kupunguza changamoto
zinazoikabili ikiwa ni pamoja na uchakavu na uhaba wa vifaa vya kisasa
ukiwemo mtandao wa Kompyuta.
Akielezea
changamoto wanazopambana nazo Mkuu wa Karakana hiyo ya Serikali Nd.
Mahmoud Hassan Khatib alimueleza Balozi Seif kwamba uhaba wa Vifaa
umekuwa ukiviza shughuli zao za kazi za kila siku.
Hata hivyo Nd.
Mahmoud alisema bado Karakana hiyo inauwezo wa kutoa huduma za vyombo
vya moto kama kawaida licha ya uhaba wa vitendaa kazi ambavyo ni vya
mtandao wa kompyuta kulingana na mabadiliko ya Teknolojia.
Alisema ushahidi wa
hayo ni ule mtiririko wa karakana za nje kupeleka vyombo walivyopewa
kuvitengeneza kumaliziwa usarifu wao katika karakana hiyo Kuu ya
Serikali.
“ Tumebahatika kuwa
na chumba kizuri cha kumalizia usarifu wa vyombo kama Magari ambacho
wenzetu wa Karakana za nje wanakitumia kwa kuleta magari yao hapa”.
Alisisitiza mkuu huyo wa Karakana Chumbuni Nd. Mahomud.
Mapema Kaimu
Mkaguzi Mkuu wa Magari Zanzibar Ndugu Masoud Saadala alisema bado wapo
maderava wakorofi wanaotumia ujanja wa kuazima mipira na baadhi ya
vipuri vya Gari zao wakati wanapopeleka kupasisha vyombo vyao.
Nd. Masoud alisema
tabia hiyo imepelekea Taasisi yao kwa kushirikiana na Idara ya Kodi na
Mapato Zanzibar { ZRB },Polisi ya Idara ya Usafiri na Leseni kulazimika kufanya Opereshani kwa lengo la kukabiliana na tabia hiyo ya hatari.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliamua kufanya ziara hiyo fupi ya
ghafla kwenye Karakana hiyo ili kujionea hali halisi ya uendeshaji wa
Taasisi hiyo muhimu kwa Serikali.
……………………..
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/7/2012.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako/ Leave your comments