TAARIFA
YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, KUFUATIA AJALI YA KUZAMA KWA MELI YA MV SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18
JULAI, 2012, CHUMBE, ZANZIBAR
Jana
tarehe 18 Julai, 2012, majira ya alasiri kumetokea ajali ya kuzama kwa meli ya
MV SKAGIT katika eneo la Chumbe, Zanzibar. Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es
Salaam kueleka Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290. Kati yao watu wazima 250,
watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.
Amiri
Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliagiza vyombo vya ulinzi na
usalama vya Serikali ya Muungano yaani JWTZ na Polisi waanze kazi ya uokoaji
mara moja.
Kazi
hiyo imefanywa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na meli za makampuni binafsi. Mpaka giza lilipokuwa limeingia na hivyo
kazi ya uokoaji kusitishwa mpaka kutakapokucha tarehe 19 Julai, 2012, watu 136
walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa zimepatikana. Aidha, mali zilizokuwa
kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa.
Kufuatia
ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano alizungumza na Dkt. Ali Mohamed Shein,
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Alimpa pole kwa ajali iliyotokea hasa kwa vifo na majeraha waliyopata Watanzania
wenzetu na watu wasiokuwa raia wa Tanzania. Alimuomba afikishe salamu za
rambirambi kwa ndugu zetu waliopotelewa na jamaa zao na kuwapa pole waliopata
majeraha na maumivu maungoni mwao.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano alisema kuwa huu ni msiba wetu sote na kwamba majonzi yao
ni majonzi yake na ya Watanzania wote. Kwa ndugu zetu waliojeruhiwa tunawaombea
kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na wapone haraka ili waweze kuendelea na
shughuli zao za kujiletea maendeleo na kulijenga taifa letu.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali
kwa uongozi wao thabiti tangu taarifa ya kutokea kwa ajali mpaka
sasa.
Aidha,
amewapongeza maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa
meli binafsi, kwa juhudi kubwa walizozifanya za uokoaji wa ndugu zetu waliopatwa
na maafa haya makubwa na ya aina yake. Amewataka waendeleze juhudi hizo leo na
siku zijazo.
Rais
amewataka wananchi wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya uokoaji
inaendelea. Kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander miezi 10
iliyopita, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali.
Kutokana
na ajali hiyo na msiba huu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa ya siku
tatu ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo, tarehe 19 Julai,
2012.
Asanteni
sana.
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
19
Julai, 2012
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako/ Leave your comments