Friday, July 20, 2012

SERIKALI YA MUUNGANO WA TANZANIA YAAHIDI KOTOA USHIRIKIANO NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KUFUATIA AJALI YA MELI YA MV SKAGIT

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema akitoa Taafifa ya uchunguzi wa awali wa Jeshi hilo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kufuatia ajali ya Meli ya M.V Skagit hapo Ofiosini Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozio Seif Ali Iddi akizungumza na Wabunge wa Muungano waliofika Zanzibar Kutoa mkono wa pole hapo katika ukumbi wa Ofisi ya Baraza la Wawakilishi Mbweni kufuatia Ajali ya Meli ya M.V. Skagit. Ujumbe huo umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mh. Shamsi Vuai Nahodha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwafariji baadhi ya Watalii na wageni waliokuwa wakija Zanzibar kwa Meli ya M.V. Skagit iliyopata ajali juzi mchana karibu na Kisiwa cha Chumbe. Kulia ya Balozi ni Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Mh. Hamad Masoud Hamad.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua baadhi ya majeruhi wa M.V Skagit waliolazwa katika Hospiotali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Ali Abdulla Ali akiwa na Makatibu wake wakitoka nje ya Ukumbi wa Baraza hilo baada ya kuahirisha kwa siku moja kikao cha baraza la Wawaklilishi jana asubuhi. Hatua hiyo imekuja kufuatia msiba uliolikumba Taifa baada ya ajali ya Meli ya M.V Skagit iliyozama karibu na kisiwa cha Chumbe. 
Picha na Saleh Masoud Mahmoud – OMPR-ZNZ. 
Serikali ya Muungano wa Tanzania Kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa litaendelea kutoa ushirikiano na msaada kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia ajali ya Meli ya M.V Skagit iliyotokea jana mchana karibu na Kisiwa cha Chumbe.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mh. Shamsi Vuai Nahodha alitoa kauli hiyo wakati akitoa mkono wa pole kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Mh. Nahodha akiuongoza Ujumbe wa Wabunge 20 wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutoa mkono huo wa pole alisema Vikosi vya Ulinzi mbali ya kusaidia operesheni hiyo pia litaendelea kuto msaada wowote utaohitajika katika kurejesha hali ya kawaida kwa wahanga hao wa ajali ya Meli.

Mh. Nahodha alisema maafa yaliyotokea jana yameigusa Jamii yote ya Watanzania hivyo Wananchi wote wanapaswa kuzidisha juhudi zao katika harakati zote za kurejesha hali ya utulivu na Amani.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru ujumbe wa Wabunge hao kwa kuguswa kwao na msiba huo uliopelekea vifo vya Watu 53 hadi sasa.
Balozi Seif alisema wazamiaji pamoja na Vikosi vya Ulinzi bado wanaendelea na operesheni ya kuwatafuta Abiria waliopotea kwenye chombo hicho.

Alisema Serikali imechukuwa gharama za mazishi kwa Mazishi ya wale wote waliokufa katika ajali hiyo sambamba na kuhudumia usafiri wa maiti ambazo Familia zao ziko Tanzania Bara.
“ Hatupendi Meli zetu zizame lakini zinazama. Hatupendi Ndege zetu zianguke lakini zinaanguka. Hiyo ni kudra ya Mwenyezi Muungu”. Alisisitiza Balozi Seif.

Hata hivyo Balozi Seif alieleza kwamba bado ipo tabia ya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wa Baharini kusaidia kufuata taratibu za usafiri zilizowekwa na mamlaka husika badala ya kutawaliwa zaidi na Tamaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa za kutembelea majeruhi wa ajali hiyo wanaoendelea kupatiwa huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Balozi Seif alielezwa kwamba jumla ya majeruhi 80 waliokuwa wamelazwa hospitalini hapo wamesharuhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata tiba.

Mmoja wa Majeruhi hao ambae ni mfanyabiashara Kitwana Makame Ali ameipongeza Serikali na Vikosi vya ulinzi kwa juhudi zao za uokozi zilizopelekea wengi kati ya wahanga hao kuokolewa.
Hata hivyo Mfanyabiashara Kitwana ameishauri Serikali kuhakikisha sheria na taratibu za usafiri wa Baharini zinazingatiwa kwa lengo la kuepusha ajali.

Baadaye Balozi Seif aliwakagua Wageni na Watalii waliookolewa ambao walikuwa wakisafiri na chombo hicho hapo katika Hoteli ya Serrena Inn Shangani Mjini Zanzibar.
Wageni hao 14 ni Paul Smeulders kutoka, Eline Van Nistelrooy,   Jaap Van Der Heyden, Joa Maouche, Inge Van Herwynen kutoka Uholanzi, Lauren Dent na Hilary Strasburg kutoka Marekani, Arne Sohns kutoka Ujerumani, Joas Gielen na Elvira Feyen kutoka Ubelgiji.
Wengine ni Bastiar Var Rennings,Lena Roker  kutoka Ujerumani Chen Dagan na Nitzan Bodenheimer kutoka Nchini Israel.

Akiwa  Ofisini kwake Vuga Balozi Seif alikutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Ispekta General Said Mwema kupokea Taarifa ya jeshi hilo tokea mwanzo wa harakati za uokozi wa janga hilo.
IGP Said mwema alimueleza Balozi Seif kwamba Jeshi la Polisi tayari limeanza uchunguzi wa awali na hitilafu kadhaa zimejichomoza kutokana na idadi halisi ya abiria waliokuwemo kwenye Meli hiyo.

Alisema mahojiano ya watu mbali mbali wakiwemo baadhi ya abiria waliokuwemo kwenye chombo hicho pamoja na wahusika wa chombo chenyewe Mjini Dar es salaam yanaendelea vyema.
Wakati huo huo Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohd Gharib Bilal amefanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Mazungumzo hayo yalikuwa katika jitihada za kutoa mkono wa pole pamoja na kutafuta mbinu za namna gani Serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana katika kukabiliana na Maafa hayo.
Dr. Bilal ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana vyema na vikosi vyote vya Ulinzi kwa jitihada zao za haraka zilizopelekea kuokoa idadi kubwa ya abiria waliokuwemo kwenye vyombo hivyo.

Dr. Bilal alimueleza Balozi Seif kwamba Serikali zote mbili ziendelee kutoa Msukumo wa msaada wa ziada kwa mamlaka zote mbili za Usafiri wa Baharini { SUMATRA na ZMA } ili kuona uimara na ukaguzi wa vyombo vya Baharini unazingatiwa vyema.
Taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imefafanua  na kuthibitisha kwamba Meli hiyo ya M.V Skagit imeruhusiwa kuchukuwa abiria 250 tuu.

 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/7/2012.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako/ Leave your comments