Wednesday, July 18, 2012

PIGO JENGINE TANZANIA! MV. STAR GATE YAZAMA KARIBU NA KISIWA CHA CHUMBE IKIWA NA ABIRIA WAPATAO 250!


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, Akitoa taarifa ya awali ya Serikali juu ya tukio la kuzama meli ya Mv. Star Gate.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakiwa katika bandari ya Zanzibar, wakisubiri bote zilizokwenda kutoa msaada katika ajali hiyo.
Boti ya ZANZIBAR 11, ikiwasili katika bandari ya Zanzibar ikiwa na abiria walionusurika katika ajali ya meli ya Mv. Star Gate.
Boti ya ZANZIBAR 11, ikiwasili katika bandari ya Zanzibar ikiwa na abiria walionusurika katika ajali ya meli ya MV. Sta Gate iliyozama leo mchana karibu na Kisiwa cha Chumbe
Meli ya Mv. Star Gate imezama karibu na Kisiwa cha Chumbe ambapo watu 12 wamefariki hadi muda huu na wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Akitoa taarifa fupi kwa waandishi wa habari,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini alisema taarifa za kuzama kwa meli hiyo ilitolewa na Boti iendayo kasi ya Kilimanjaro III iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar ndipo ilipoiona meli hiyo ikizama.

“Tulipata taarifa kutoka Boti ya abiria ya Kilimanjaro III saa 7:50 mchana waliporipoti kuona meli ikizama karibu na Kisiwa cha Chumbe” Alisema Waziri Mwinyihaji.

Waziri huyo alisema Meli hiyo imezama maili sita kuelekea Kisiwa cha Yasin Kusini mwa Kisiwa cha Chumbe kilichopo Unguja maili kadhaa kutoka Bandari ya Malindi.

Waziri Mwinyihaji alisema idadi ya abiria walikuwa 250 ambao ni watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6. “Tumepeleka waokoaji, kuna boti tano zipo eneo la tukio kushirikiana na waokoaji wengine” Alisema Waziri Mwinyihaji.

Alisema maiti zote zitapelekwa viwanja vya Maisara Zanzibar kwa ajili ya ndugu na jamaa kuzitambua maiti za ndugu zao ambapo majeruhiwa wote watatibiwa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.

Katika Bandari ya Malindi kumeshuhudiwa maiti kadhaa zikiwemo za watoto zikishushwa, Miongoni mwa abiria waliookolewa ni raia 13 wa Mataifa mbalimbali ya nje huku raia mmoja ambaye hakuweza kutambuliwa utaifa wake  amepoteza maisha.

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alifika eneo la Bandari ya Malindi Zanzibar pamoja viongozi wengine akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Mawaziri na  baadhi ya Wajumbe a Baraza la Wawakilishi walikuwepo kutoa msaada  unaohitajika.

Katika eneo la pembezoni mwa bandari ya Malindi, makundi ya wananchi yalikuwa yamekusanyika wakisubiri taarifa za tukio hilo tangu saa 8:30 mchana.
Meli ya Mv. Star Gate inamilikiwa na kampuni ya kizalendo ya Sea Gull Sea Transport Ltd ambayo mwaka 2009 Meli yake nyengine ya Mv. Fatih ilipinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi Zanzibar na kua watu sita.

Mwaka jana Zanzibar ilikumbwa na maafa baada ya Meli ya Mv. Spice Islanders kuzama katika bahari ya Hindi eneo la Nungwi katika Kisiwa cha Unguja ikielekea Kisiwani Pemba ambapo taarifa rasmi ya Serikali ilisema watu 197 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.

Ali Mohamed (Mkurungenzi wa Fitna)

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako/ Leave your comments