Thursday, July 19, 2012

TAARIFA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, KUHUSU AJALI YA MELI YA MV SKAGIT YA KAMPUNI YA SEAGUL JULAI 18, 2012

BISMILLAH RAHMAN RAHIM
 
Ndugu Wananchi,
 
ASSALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH
 
Kwa masikitiko makubwa leo Jumatano, Julai 18, 2012 nchi yetu imepata tukio la huzuni kubwa la ajali ya kuzama meli ya mizigo na abiria ya MV SKAGIT tukio ambalo limesababisha vifo, majeruhi na kupotea mali za watu.
 
Ajali hiyo imetokea wakati meli hiyo ilikuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar.  Taarifa za awali za MV SKAGIT ni kuwa meli hio ilikuwa  na jumla ya watu 290. Kati ya hao wafanyakazi ni watu 9, abiria watu wazima ni 250 na watoto 31.  Meli hiyo ilipata maafa hayo maeneo ya Kisiwa cha Chumbe milango ya saa nane mchana.  Mara baada ya taarifa ya ajali hiyo kutufikia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikishirikiana na taasisi mbali mbali zikiwemo Idara Maalum za SMZ, Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mamlaka ya Usafiri wa Baharini pamoja na vyombo vya usafiri wa baharini vya watu binafsi na wananchi kwa jumla  ilichukua hatua za haraka kufika eneo hilo kwa kazi za uokozi.
 
Mpaka saa za magharibi hivi leo, idadi ya watu waliookolewa 136 na maiti 31 wamepatikana, wakiwemo watu wazima 24 akiwemo raia wa kigeni mmoja na watoto 7.  Jumla ya watu 123 bado hawajaonekana.  Juhudi za uokozi ziliendelea hadi kuingia giza na zitaendelea mara kukipambuzuka.  Hali ya bahari ilikuwa mbaya wakati huo na meli hiyo ilipinduka katika mawimbi makubwa.
 
Ndugu Wananchi,
Tukio hili ni msiba mkubwa kwa wananchi wote wa Zanzibar na taifa la Tanzania kwa jumla. Ni wakati mgumu kwetu sote na napenda kutoa wito kwa watu wote tuwe na subira na wastahamilivu.  Huu ni wakati wa kufikiria ndugu na watoto wetu waliopoteza maisha yao na tuwatakie rehema za Mola wetu.  Aidha, tunawaombee nafuu waliopata majeraha.
 
Kwa niaba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar natoa pole kwa wafiwa wote na namuomba Mwenyezi Mungu awape subira.  Kwa wale ambao bado hawajapata taarifa za watu wao waliokuwa katika safari hiyo, nawaomba wawe wavumilivu wakati tunafanya juhudi zote za uokozi na utafutaji miili ya waliofariki.
 
Vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi mbali mbali vitaendelea kuchukua kila hatua inayofaa katika kazi hiyo. Natoa shukurani zangu na za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wenye vyombo vya bahari binafsi vilivyoshiriki katika kazi za uokozi na kuokota maiti na pia wananchi wengine waliojitolea. Kadhalika, navishukuru vyombo vya habari kwa kuendelea kuwaarifu wananchi tukio hili kila hatua.  Ni matumaini yetu kwamba wataendelea kushirikiana na sisi katika kushughulikia tokeo hili.
 
Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia gharama zote za mazishi ya wale waliofariki na pia itatoa huduma ya afya, matibabu na nyengine kwa wote waliopata majeraha.  Tutatangaza mipango yote kupitia vyombo vya habari na njia nyengine.
 
Kutokana na msiba huu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatangaza siku tatu za maombolezi kuanzia kesho tarehe 19 Julai, 2012.  Katika kipindi hicho sherehe na tafrija zote zinazatakiwa kusitishwa.  Bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
 
Nawasihi wananchi kuwa huu si wakati wa kutupiana lawama au kueneza habari zisizothibitishwa.  Sote tushirikiane na kusimama pamoja katika tukio hili la msiba na maafa.  Tukubali kuwa msiba huu ni amri ya Mwenyezi Mungu na umeandikwa kuwa mtihani kwetu.  Mola wetu anatuambia kuwa binadamu tutapewa mitihani ya kupoteza maisha na mali.  Huu ni mtihani mmojawapo wa hiyo.  Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe subira.
 
Ina Lillahi Waina Ilayhi Rajiiun. 

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako/ Leave your comments