Na
Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar
Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Julai 19 hadi
Julai 21 kufuatia maafa ya ajali ya Meli ya Mv. Skagit iliyozama karibu na
Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein
akitangaza maombolezo hayo, alisema bendera zote zitapepea nusu mlingoti na
kwamba shughuli za sherehe na burudani zimefutwa kwa muda wa siku tatu za
maombolezo.
Dk.
Shein alisema shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida. Katika taarifa yake
aliyoitoa Ikulu usiku wa kuamkia Julai 19, Rais Dk Shein amewahakikishia
wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba gharama zote za
mazishi na pia kugharamia huduma za matibabu kwa majeruhi.
“Nimesikitishwa
sana na msiba huu, Katika wakati huu si vema tukaanza kulaumiana jambo la muhimu
hivi sasa ni kuokoa maisha ya watu” Alisema Rais Dk. Shein.
Mbali
ya taarifa hiyo, Rais Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi wa Serikali,
vyama vya siasa, Viongozi wa dini katika kutambua maiti zilizofikishwa katika
eneo maalum la viwanja vya Maisara Suleiman.
Mbali
ya kwenda katika viwanja hivyo, pia alifika katika eneo la bandari ya Zanzibar
kufuatilia taarifa za tukio hilo. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana
lilisitisha shughuli zake kufuatia maafa hayo ambapo wakati wa jioni Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi alitarajiwa kufanya majumuisho ya
bajeti yake.
Baadhi
ya Wabunge wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Shamsi Vuai
Nahodha, Mkuu wa Jeshi la Polisi walitembelea majeruhi katika Hospitali Kuu ya
Mnazi Mmoja pamoja na eneo la viwanja vya Maisara ambapo maiti hufikishwa kwa
ajili ya utambuzi.
Mbali
ya Bunge, pia Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana lilisitisha kwa muda shughuli
zake ili kutoa nafasi kwa Wawakilishi hao wa wananchi kushiriki katika shughuli
za uokozi ambapo wengi walifika bandarini kusaidia kazi mbalimbali ikiwemo
kuwafariji waliopoteza ndugu zao.
Taarifa
kutoka Mamlaka za Serikali zinaeleza kwamba hadi asubuhi hii maiti 30
zilipatikana ambapo 20 kati ya hizo zimetambuliwa na kuchukuwa na jamaa zao huku
wananchi wengine wakiendelea na kuzitambua maiti zinazofikishwa katika eneo la
Maisara.
Aidha,
katika taarifa hiyo, watu 145 wameokolewa wakiwa hai, wengi wao wapo katika hali
nzuri wameruhusiwa kuungana na familia zao baada ya kupatiwa matibabu katika
Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar.
Meli
ya Mv. Skagit ilizama Julai 18,2012 saa 7:50 mchana ikitokea Bandari ya Dar es
Salaam kwenda Zanzibar ikiwa imebeba abiria 250 watu wazima, watoto 31 na
mabaharia 6.
Kazi
ya utafutaji na uokoaji zinaendelea asubuhi hii katika eneo la tukio ilikozama
meli hiyo umbali wa maili sita Kusini mwa Kisiwa cha Yasin karibu na Kisiwa cha
Chumbe Zanzibar.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako/ Leave your comments