Tuesday, July 17, 2012

MAKAMU WA PILI WA RAISI WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI ATEMBELEA KARAKANA KUU YA SERIKALI ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akielezea umuhimu wa kuimarishwa kwa Karakana Kuu ya Serikali iliyopo Chumbuni mbele ya Mkuu wa Karakana hiyo Nd. Mahmoud Hassan Khatib kufuatia ziara yake ya ghafla kwenye Karakana hiyo.
Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Magari Zanzibar Nd. Masoud Saadala akielezea changamoto zinazoikabili Taasisi yao katika utekelezaji wa kazi zao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara ya ghafla katika karakana Kuu ya Serikali iliyopo Chumbuni Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipata maelezo ya utendaji kazi kutoka kwa wahandisi wa Karakana Kuu ya Serikali iliyopo Chumbuni  kutoka kwa Mkuu wa Karakana hiyo Nd. Mahmoud Hassan Khatib.

Serikali kupitia Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano inakusudia kuijengea uwezo zaidi Karakana Kuu ya Serikali kwa lengo la kuirejeshea hadhi yake ya kutoa huduma za kitaalamu zaidi.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara ya ghafla katika Karakana hiyo iliyopo Mtaa wa Chumbuni Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema haipendezi kuona vyombo vya Moto hasa vile vya Serikali vinapelekewa kupata huduma ya kiufundi katika Karakana binafsi wakati ile iliyowekwa Maalum na Serikali kwa ajili ya Vyombo hivyo inakiukwa.

Alisema mpango huo ambao sio utaratibu unaokubalika  Kiserikali unaweza kutoa mwanya  kwa baadhi ya watendaji wa Serikali kutumia vibaya Fedha za Umma katika utengenezaji wa vyombo hivyo. 

“ Haitoi sura nzuri kuona Maafisa wa Taasisi za Umma wanaamua kupeleka magari yao katika karakana za nje wakati ile ya Serikali ipo kwa ajili ya shughuli hiyo”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa Karakana hiyo kwamba lile ombi lao lililopelekwa ngazi ya juu kwa ajili ya kupatia ufumbuzi litaangaliwa Serikalini na kupatiwa ufumbuzi unaofaa.

Alisema hatua hiyo itaweza kusaidia kwa njia moja Karakana hiyo kupunguza changamoto zinazoikabili ikiwa ni pamoja na uchakavu na uhaba wa vifaa vya kisasa ukiwemo mtandao wa Kompyuta.

Akielezea changamoto wanazopambana nazo Mkuu wa Karakana hiyo ya Serikali Nd. Mahmoud Hassan Khatib alimueleza Balozi Seif kwamba uhaba wa Vifaa umekuwa ukiviza shughuli zao za kazi za kila  siku.

Hata hivyo Nd. Mahmoud alisema bado Karakana hiyo inauwezo wa kutoa huduma za vyombo vya moto kama kawaida licha ya uhaba wa vitendaa kazi ambavyo ni vya mtandao wa kompyuta kulingana na mabadiliko ya Teknolojia.

Alisema ushahidi wa hayo ni ule mtiririko wa karakana za nje kupeleka vyombo walivyopewa kuvitengeneza kumaliziwa usarifu wao katika karakana hiyo Kuu ya Serikali.
“ Tumebahatika kuwa na chumba kizuri cha kumalizia usarifu wa vyombo kama Magari ambacho wenzetu wa Karakana za nje wanakitumia kwa kuleta magari yao hapa”. Alisisitiza mkuu huyo wa Karakana Chumbuni Nd. Mahomud.

Mapema Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Magari Zanzibar Ndugu Masoud Saadala alisema bado wapo maderava wakorofi wanaotumia ujanja wa kuazima mipira na baadhi ya vipuri vya Gari zao wakati wanapopeleka kupasisha vyombo vyao.

Nd. Masoud alisema tabia hiyo imepelekea Taasisi yao kwa kushirikiana na Idara ya Kodi na Mapato Zanzibar { ZRB },Polisi ya Idara ya Usafiri na Leseni  kulazimika kufanya Opereshani kwa lengo la kukabiliana na tabia hiyo ya hatari.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliamua kufanya ziara hiyo fupi ya ghafla kwenye Karakana hiyo ili kujionea hali halisi ya uendeshaji wa Taasisi hiyo muhimu kwa Serikali.
  
……………………..
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/7/2012.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako/ Leave your comments